Linapokuja swala zima la kupanga nyumba ni wazi kuwa unahitaji kuwa makini sana kwani kwa kuchagua nyumba ambayo sio sahihi unaweza kuharibu maisha yako kwa muda, na hata kupoteza pesa pia.
Kuliona hili leo nimekuletea makala fupi ambayo inaweza kukusaidia kujua vitu vya kuangalia kabla ya kupanga nyumba yoyote. Basi bila kupoteza muda twende moja kwa moja.
Eneo ilipo Nyumba
Niwazi kuwa ni muhimu kuchagua nyumba ambayo inaendana na mazingira ambayo pengine wewe unahitaji, ndio maana ni muhimu kujua kwanza unataka nyumba eneo gani.
Hapa sio kuangalia eneo pekee, ni pamoja na mtaa, kitongoji pamoja na nyumba imepakana na vitu vya aina gani. Hii ni muhimu sana kwani kumbuka eneo hilo ndipo utakapo ishi kwa miezi sita au zaidi.
Historia ya Nyumba na Eneo Ilipo
Unaweza kudhani jambo hili sio la muhimu lakini ni jambo la muhimu sana hasa kama unayo familia au unaishi na ndugu na jamaa. Baadhi ya maeneo huwa na historia mbaya na pia wakati mwingine migogoro ambayo baadae inaweza kusababisha usumbufu wa kuhama bila kutarajia.
Unaweza usipate historia ya eneo husika kwa haraka hivyo ni muhimu kuchukua muda wako kutafuta watu au majirani ambao wataweza kukwambia historia ya eneo husika ikiwa pamoja na wapangaji au mpangaji aliyetoka kabla yako.
Hakikisha unafanya hivyo kabla ya kuhamia kama unaweza unaweza kuuliza mwenye nyumba (japo kuwa wengi hawasemi ukweli, hivyo tafuta sehemu kama za maduka ya karibu eg, kwa mangi kisha muulize muuza duka wengi huwa na historia za nyumba nyingi mtaani.)
Mfumo wa Maji Safi na Maji Taka
Watu wengi sana wanasahau kuangalia mfumo wa maji taka kuliko mfumo wa maji safi, ni muhimu sana kuangalia mifumo yote miwili hii ikiwa pamoja na sehemu za kuhifadhi maji taka na idadi ya watu ambao hutumia mfumo huo.
Mifumo ya maji ambayo sio imara inaweza kusababisha usumbufu mkubwa sana hasa pale ambapo unatumia choo zaidi ya kimoja hivyo ni muhimu sana kuhakikisha kama vyoo vyote vinaflash vizuri na maji hayasimami kwa namna yoyote.
Pia mfumo wa maji safi ni muhimu sana hivyo hakikisha unajua unapata wapi maji safi na kama ni sehemu ya kudumu, usikubali kama umeambiwa maji yanapatikana hapo nyumba ya jirani.!
Chumba au Nyumba Yenyewe
Ni muhimu kuangalia kwa makini sana nyumba yenyewe hii ikiwa pamoja na na madirisha ya nyumba, ukuta na sehemu zote za muhimu kama vyumba na milango.
Ukuta
Hakikisha kuta zote ni kavu kwa asilimia 100 na hazi hifadhi unyevu na ziko salama, kama kuna sehemu yoyote unaona haipo sawa hakikisha unaomba marekebisho kabla ya makubaliano yoyote. Hakikisha una angalia kuta zote za nje na ndani.
Madirisha
Kwa upande wa madirisha hakikisha madirisha yapo imara na yenye ulinzi wa kutosha hii ni pamoja na vioo, nyavu za kuzuia mbu, pamoja na usalama wa madirisha yenyewe ni muhimu sana hasa kama eneo unapoishi upo karibu na sehemu yoyote ya mkusanyiko wa watu.
Paa la Nyumba
Paa la nyumba husika hakikisha halivujishi maji kwa namna yoyote na unaweza kujua hili kwa kuangalia siling board ya nyumba kama ina alama zozote za kuashiria kuvuja, kama umeona sehemu yoyote ya namna hiyo hakikisha unauliza na unahitaji marekebisho kabla ya kuamia.
Milango
Milango yote ya nyumba hakikisha inafunga kwa funguo na pia kuna milango ya chuma kwa ajili ya usalama hasa kwa milango ya nje. Nyumba isiyo na milango ya chuma mara nyingi huwa na usalama mdogo na huvutia wezi.
Sakafu
Hakikisha sakafu ya nyumba husika haifadhi unyevu na ipo imara, usikubali nyumba yenye sakafu iliyopasuka au yenye unyevu kwani hiyo ni ishara ya kuvuja kwa paa na kusababisha sakafu kwa na unyevu muda wote na hatimae kuvunjika.
Usalama wa Chumba au Nyumba
Kwa kumalizia ni muhimu sana kuangalia usalama wa eneo husika, hii ni pamoja na geti, majirani pamoja na watu unao ishi nao. Ni vyema kuangalia haya kabla ya kuhamia kwani unaweza kujikuta unaishi sehemu isiyo na usalama hasa kama hautakuwa makini na vitu hivi.
Pia kuangalia majirani ni muhimu, kwani hata watu wabaya nao pia wanapanga kwenye nyumba hizo hizo ambazo kila mtu hupanga. Kama inawezekana, ni vyema kuchagua sehemu yenye familia kuliko mtu mmoja mmoja.
Serikali za Mitaa
Jambo la mwisho kabisa hakikisha unajua mjumbe wako anapoishi na mahali ofisi za serikali za mitaa zilipo hii itakusaidia sana hasa pale unapo pata matatizo kwa namna yoyote ile.