Ni gharama kubwa kutafuta wateja wapya kuliko kuwafanya wale ulio nao tayari wabaki kwako. Hivyo ni lazima uwathamini na uwajali wateja ulionao.
Unahitaji kuwafanya wateja wako wawe na furaha. Unahitaji kuwafanya wawe wateja wanaokuja kwako kila mara na waweze kuleta marafiki zao. Kama utakuwa na wateja wasio na furaha, wanaweza wakasambaza maneno ya sio mazuri kuhusu biashara yako kwa watu wengine.
Sasa unafanya nini kuhakikisha wana furaha na biashara yako? Jaribu njia hizi saba za kuwafanya wateja wako wapende wanachopata kutoka kwako.
1. Jifunze Kuhusu Wateja Wako
Ili kufanya wateja wako kupenda biashara yako, kwanza unahitaji kujua wanachotaka. Anza kwa kutafuta wateja wako wanataka nini kwa kuchunguza nini kipo sokoni na nini hakipo.
Wakati wa kuchunguza kuhusu soko, unatakiwa kutafuta kujua juu ya mahitaji, matakwa, maslahi na idai ya wateja wako. Ukijua wanachotaka, utaweza kuwapa. Mfano, kama umetafiti na kugundua sehemu fulani kuna uhaba wa viatu vya ngozi, ni rahisi kuanzisha biahsara hivyo na kupata watu. Wateja wakipata wanachotaka, lazima wafurahi, lazima wathamini biashara yako.
2. Kuwa na Uvumilivu
Wateja hawatapenda unachofanya kila wakati. Ni kawaida na mara zote wateja kuwa na matatizo na bidhaa tofauti. Hata wote tumewahi kuwa wateja na tukalalamika sehemu kuhusu bidhaa fulani.
Cha muhimu, wakati mteja atakapokuja kukulalamikia kitu, uwe mvumilivu. Ni rahisi kutupilia mbali madai yake kuhusu bidhaa zako na hata kumfukuza. Lakini, chukua muda wa kumsikiliza mteja. Kuwa na subira nao na usikilizee kila kitu wanachosema. Hata kama wanalalamika kitu ambacho hakihusiani na wewe. Uvumilivu ni sehemu ya huduma nzuri kwa wateja.
Baada ya mteja kumaliza kueleza malalamiko yake, basi unaweza kumjibu. Zingatia kuwa, usimfanye ajione kuwa mawazo yake hayana msingi. Kumbuka, mteja mara zote yuko sahihi.
3. Usiwachukulie kama Wateja, Wafanye Marafiki
Unaweza kujuana na kuwa na uhusiano binafsi na wateja wako. Ongea na wateja wako kama wao ni marafiki wako. Hata kama hauna uhusiano wa moja kwa moja na wateja, bado unaweza kuongeza uhusiano wa kibinafsi kati ya biashara na wateja wako. Unaweza kutumia majina yao katika barua pepe. Pia unaweza kushirikiana na wateja wako katika mitandao ya kijamii.
Cha kuzingatia, ikiwa unataka kuwa na uhusiano wa kibinafsi na wateja, usiwe roboti. Usitume majibu ya ki-automatiki kwa wateja wako wa karibu. Hakuna mteja atakayefurahi kukutumia ujumbe kisha akajibiwa na ujumbe wa ki-automatiki uliosetiwa katika kompyuta. Tafuta njia za kuonyesha tabia ya biashara yako na ujumuishe wateja ndani yake, hata ikiwa katika ujumbe unaowatumia.
4. Toa Ofa na Madili ya Kuvutia
Watu wengi wanapenda madili kama vile punguzo la bei na ofa. Wateja wakiona wanapata thamani za pesa zao katika madili na ofa za bidhaa zako, watakuwa na uwezekano mkubwa wa kurudi.
Unaweza kutoa punguzo na madili mengine katika sherehe za msimu wa mwaka. Au unaweza kutoa bidhaa za bure kwa wateja wazijaribu, au ile ya nunua-moja-upate-moja bure. Uuzaji huo huhamasisha wateja kuendelea kurudi kwenye biashara yako. Wakati watu wanapenda madili na punguzo katika bidhaa zako, watapenda biashara yako zaidi.
Hata kama ofa na madili yanaweza kukusababisha usipate faida kwa sasa, lakini mauzo kwa wateja wanaojirudia kila mara yataongeza msingi wa biashara yako siku za mbeleni.
Hakikisha utangaza madili haya kwa wateja wako. Mbinu hii inafanya kazi tu ikiwa wateja wanajua juu ya madili na ofa unazotoa kwa ajili yao.
5. Anzisha Mfumo wa Wateja Waaminifu
Pia unaweza kujaribu kuanzisha programu kwa wateja waaminifu kwenye biashara yako. Kwa mfano, mteja anaweza kupata punguzo au vitu vya bure baada ya kutumia kiasi fulani au kutembelea biashara yako idadi fulani ya siku. Kuna migahawa Dar es Slaaam, ilikua inatoka vinywaji na vyakula bure kwa kila mteja atakaye rudi mara ya tatu katika mgahawa huo.
Programu ya uaminifu kwa biashara ndogo huwapa wateja motisha ya kuendelea kurudi kwenye biashara yako. Na wanapopata zawadi kwa kuwa wateja waaminifu, watajisikia vizuri. Hii ni njia rahisi kufanya wateja kuhisi unawanajali.
6. Wajuze Wateja Wako
Mara zote, ongea na kuwa wazi kwa wateja wako. Kila mara wakati biashara yako ina habari au matukio mapya yanayowagusa wateja, wajulishe. Waeleze kuhusu vitu vya kuvutia na kufurahisha vinavyoendelea ili kuwatengeneza msisimko.
Pia, waambie wateja wako juu ya mambo mabaya, kama vile kuhusu uhaba wa bidhaa na ucheleweshaji. Mfano, kama siku ulikuwa unawafanyia ‘delivery’ na ukakwama njiani, hakikisha unatoa taarifa mapema kabla wao hawajakutafuta. Kuwa mwaminifu juu ya kila kinachotokea ndani ya biashara yako.
Wateja watathamini uaminifu wako. Watakufurahia wakati mambo mazuri yatatokea na kuwa na uelewa wakati mambo mabaya yanatokea.